Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amekubali kuachia madaraka ya kuongoza nchi hiyo, baada ya wito uliotolewa na chama chakle ANC kumtaka kujiuzulu ndani ya masaa 48.

Makubaliano hayo ya kujiuzulu yamekuja na sharti kwamba atafanya hivyo baada ya miezi mitatu mpaka sita kuanzia sasa, na bado uongozi wa ANC haujatoa jibu kama umeridhia ombi hilo.

Hapo jana chama cha ANC kikiongozwa na Cyril Ramaphosa ambaye alichukua wadhifa wa Zuma wa kukiongoza chama hiko, kilituma ujumbe maalum kumtaka rais huyo kuachia madaraka, kutokana na harakati nyingi za kumtaka afanye hivyo tangu mwaka jana.

Jacob Zuma anakabiliwa na tuhuma za rushwa, na Bunge la nchi hiyo kujaribu kupiga kura za maoni ili kumuondoa lakini ilishindikana, na ndipo chama kuamua kuchukua uamuzi huo mgumu wa kumtaka afanye hivyo, la sivyo kitamtoa kwa nguvu.

Iwapo Zuma atafanya hivyo atakuwa amefuata nyayo alizopita rafiki yake mkubwa Robert Mugabe ambaye alikuwa Rais wa Zimbabwe, aliyetakiwa kufanya hivyo mwishoni mwa mwaka 2017 na jeshi la nchi hiyo, la sivyo lingetumia nguvu kumng'oa, na hatimaye kuachia madaraka.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: