WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametangaza kuanza kwa awamu ya pili ya operesheni ya kupambana na kudhibiti uvuvi haramu na utoroshaji wa samaki na mazao yake katika Ziwa Victoria.

Aidha, Mpina amemwagiza Katibu Mkuu wa Uvuvi wizarani kwake, Yohana Budeba, na Halmashauri kuwasimamisha kazi watumishi 35 wa idara ya uvuvi waliobainika kushiriki na kufadhili uvuvi haramu na kuagiza uchunguzi uanze mara moja ili waweze kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Akizungumza katika kikao cha tathmini ya operesheni sangara 2018 awamu ya kwanza iliyoanza Januari mosi hapa jijini Mwanza, Waziri Mpina alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa nguvu zote kupambana na uvuvi haramu.

Mpina alisema awamu ya kwanza ya operesheni hiyo iliyoshirikisha viongozi kutoka Idara ya Uvuvi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Jeshi la Polisi na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Hifadhi ya Mazingira (NEMC), imekusanya Sh. bilioni 4.7 kama faini kutoka kwa watu wote waliobainika kuhusika na uvuvi haramu.

Alisema faini hizo zilitozwa kwa wavuvi, viwanda 11 vya kuchakata minofu ya samaki vilivyokutwa na samaki wasioruhusiwa, viwanda vitatu vya nyavu  haramu pamoja na wafanyabiashara 16 wa kuuza nyavu haramu.Pia alisema nyavu 395,000 zenye thamani ya mabilioni ya shilingi ziliteketezwa kwa moto.

Alisema operesheni hiyo mbali na kupewa baraka na Ilani ya uchaguzi ya CCM pia inatekelezwa kwa kufuata sheria mbalimbali.

Waziri Mpina alitumia fursa hiyo ya mkutano kuwakumbusha viongozi wa ngazi zote kuzingatia viapo vyao vya maadili ya utumishi wa umma katika kusimamia rasilimali za taifa.

Alitolea mfano mwaka jana kilo milioni nne za samaki aina ya kayabo zilitoroshwa kwenda nchi za Malawi na Zambia kupitia mipaka iliyoko mkoa wa Songwe huku viongozi wa ngazi zote wakiwepo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: