JESHI la Polisi mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana  na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) mkoani hapa  imemkamata Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Misungwi Bw. Anthony Bahebe.
 
Pia Mwanasheria wa Halmashauri hiyo Bw. Alphonce Sebukoto naye amekamatwa na Jeshi hilo. Viongozi wote hao wanakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na ubadhilifu wa fedha za umma.
 
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema kukamatwa kwa viongozi hao kunatokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.
 
Kamanda Msangi alisema, Bw. Sebukoto alikamatwa Februari 19, 2017 na Bw. Bahebe amekamatwa leo na wote wanaendelea kuhojiwa na Polisi kwa kushirikiana na TAKUKURU.
 
Naye Kamanda wa TAKUKURU wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Ernest Makale alisema Bw. Sebukoto aliidhinisha malipo ya sh.milioni 278 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Bahebe.

Alisema Bw. Sebukoto aliidhinisha malipo hayo kwa Bw. Bahebe Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya ukurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi ambapo jumla sh. milioni 138 ziliingizwa katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti huyo. Alisema kiasi kingine cha fedha kinachunguzwa kubaini kilipo.

Kukamatwa kwa viongozi hao kunatokana na juhudi za Serikali katika mapambado dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka pamoja na fedha za umma.
 
Februari 19, 2019 akiwa katika ziara yake wilayani Misungwi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Misungwi Bw. Sebukoto na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.
 
Alichukua hatua hiyo baada Mwanasheria huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kushindwa kuishauri vyema halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya sh. milioni 278.

Amesema Mwanasheria huyo Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya ukurugenzi aliidhinisha malipo ya sh.milioni 278 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Anthony Bahebe.

Waziri Mkuu alisema Bw. Bahebe aliishtaki halmashauri hiyo akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi ya ukandarasi wa mradi wa maji Igenge uliojengwa na kampuni ya ukandarasi ya Seekevim.

Alisema mradi huo ulianza 2014 na ulitakiwa ukamilike 2015. Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo hayo wakati ambao tayari hati maalumu ya uwakilishi ilikuwa imekwisha tangu Desemba 2015.

Alisema Mwanasheria alimlipa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri jambo ambalo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Hivyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao.

  (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 21, 2018.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: