KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema ni marufuku kwa mwanachi yoyote kushiriki kwenye maandamano kwani hawapo tayari kuona watu wakiandamana na kusababisa uvunjifu wa amani iliyopo.

Mambosasa ametoa kauli hiyo jana  jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia mambo mbalimbali na ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kutojihusisha na maandamano.

Alifafanua kwenye mitandao ya kijamii kuna baadhi ya watu wanaitumia vibaya na sasa wameanza kuhamasisha maandamano kwa kupanga tarehe ambayo itakuwa Aprili 26 mwaka huu.

“Kwenye mitandao ya kijamii tumeona watu wanahamasisha maandamano.Tunawaambia Polisi hatutakaa kimya na wale ambao wataandamana kitakachotokea wasitulaumu.

“Polisi tumejipanga kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na wanafurahia hali ya ulitulivu iliyopo.

"Wale ambao wanataka kufanya maandano wahesabu hawana bahati na ndio maana tunaomba wananchi wasishiriki kwenye maandamano ambayo yameanza kuhamasishwa kupitia mitandao ya kijamii,”alisema Mambosasa.

Alifafanua Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linataka kuona wananchi wakiendelea na shughuli zao za kimaendeleo na wachache wenye kutaka kuvuruga amani iliyopo haitawavumilia.

Hivi karibuni kumekuwa na vuguvugu la kufanyika maandamano  Aprili 26 huku Mwanaharakati wa mitandaoni Mange Kimambi akionekana kuwa mstari wa mbele katika uhamasishaji.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: