Mtafaruku umezuka kwenye kikao cha Baraza maalum la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilayani Hanang' Mkoani Manyara

Mtafaruku huo ni baada ya wajumbe kupinga kitendo cha Mwenyekiti wa UVCCM wa Wilaya hiyo Ester Mchome kutaka kupitisha kwa mabavu jina la Katibu wa hamasa na chipukijzi wa Wilaya hiyo Joelina Pareso bila ridhaa ya wajumbe hao. 

Tukio hilo limetokea leo Februari 20 katika kikao hicho kilichofanyika , Katesh makao makuu ya wilaya hiyo na kusababisha Mwenyekiti huyo afunge kikao mara mbili baada ya kukifunga mara ya kwanza kwa hasira na kutoka nje. 

Mjumbe wa baraza la UVCCM wilaya hiyo Mwinyi Bajuta alipinga utaratibu uliotumika kupitisha jina hilo kwani vijana hawaungi mkono uteuzi huo hivyo litafutwe jina lingine tofauti na hilo.

"Mimi na wewe tuligombea hiyo nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya na wewe ukapata kwa nini hutaki kuvunja makundi tujenge jumuiya," amesema  Bajuta. 

Mjumbe mwingine Emmanuel Gamasa alisema ni vyema kanuni na utaratibu ukafuatwa ili kupatikana kwa jina lenye mashiko tofauti na hali inavyokwenda kwenye jumuiya hiyo kwa sasa. 

"Jumuiya ni yetu na tunapaswa kuipeleka vizuri hadi tufikie malengo yetu Mwenyekiti, hilo jina wajumbe hawalikubali wewe using'ang'anie kulipitisha," amesema Gamasa. 

Naye mjumbe Yohani Leonce amepinga  utaratibu wa kupitisha majina ya wajumbe wa kamati ya utekelezaji wa wilaya hiyo kwani wengine waliteuliwa lakini hawajahudhuria vikao vitatu tangu wapewe nafasi hizo. 

"Hizi nafasi za kupeana kwa kujuana madhara yake ndiyo kama haya mnamteua mtu kumbe hawezi kufanikisha majukumu mnayompa faida yake ni nini kama siyo ubabaishaji?" amehoji Leonce. 

Hata hivyo, Mchome ameridhia hitaji la wajumbe hao na kupanga upya kikao kijacho Machi 4 kitakachoteua mwanachama mwingine kuwa katibu wa hamasa na chipukizi wa wilayani hiyo.

Mchome amesema wanapaswa kuanza upya ili kuhakikisha wanaijenga UVCCM Hanang' yenye nguvu, umoja, imara na mshikamano kwani wao ndiyo dira ya chama. 

"Leo mmenifundisha jambo kubwa, nami napenda kukosoa na kukosoana, Mwenyekiti wenu anawapenda sana, tukutane mwezi ujao kwenye baraza la kawaida," amesema Mchome. 


Share To:

msumbanews

Post A Comment: