Polisi wa Uganda wawazuilia wanahabari wa gazeti la Daily Monitor kuondoka afisini zao mjini Kampala kwa tuhuma kwamba gazeti hilo liliandika tahariri ya kuikashfu serikali.
Chama cha waandishi wa habari nchini Uganda kinalaani ongezeko la ukamatwaji kiholela wa Waandishi nchini humo na Jeshi la Polisi kisha kufunguliwa kesi za uhaini na wengine kutekwa na watu wasiojulikana kisha kupelekwa magerezani bila kufikishwa mahakamani.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana na chama hicho imejiri baada ya waandishi wa habari watatu wa gazeti wa Daily Monitor kukamatwa katika mazingira ya utatanishi na kushtakiwa kwa njama ya kujaribu kuipindua serikali, mashtaka ambayo adhabu yake ni kifo endapo watakutwa na hatia.
Nchini Uganda kumekuwa na ripoti za waandishi wa habari kutekwa na watu wasiojulikana na kisha baadaye kupatikana gerezani wakiwa wamefungwa bila hatia kumezua hofu kubwa kwa waandishi wa habari.
Jana Jumatatu Februari 19, 2018 mwandishi wa habari wa kituo cha habari cha kibinafsi cha Top Radio, Richard Kasule alikamatwa nje ya ofisi za kituo hicho muda mfupi baada ya kuandaa matangazo ya asubuhi.
Wafanayakazi wenzake katika kituo hicho cha habari walidai kwamba Kasule alikamatwa na polisi baada ya kufichua ushirikiano kati ya walinda usalama na makundi ya uhalifu jijini Kampala.
Mtangazaji huyo aliandaa kipindi cha saa nzima akiwahoji viongozi wa makundi hayo ya uhalifu waliodai kushirikiana na polisi katika uhalifu.
Hatua ya kukamatwa kwa kasule inajiri siku mbili baada ya mwandishi wa gazeti la serikali la the New Vision, Charles Etukuri, kukamatwa nje ya ofisi za gazeti hilo la serikali.
Etukuri alichapisha taarifa ya upekuzi kuhusiana kifo cha mwekezaji kutoka bara la Ulaya katika hoteli moja maarufu jijini Kampala, na kukamatwa kwa viongozi wakuu 6 wa polisi kisiri.
Mwandishi mwingine wa habari, Isaac Bakka, alipatikana gerezani baada ya kutoweka katika mazingira ya kutatanisha wiki mbili zilizopita.
Hata hivyo, Mahakama jijini Kampala kupitia Mkurugenzi wa Habari, Solomon Muyita, amesema mwandishi huyo alikuwa ameshafunguliwa mashtaka ya uagizaji wa silaha hatari kwa nia ya kuipindua serikali ya Yoweri Museveni.
Wahariri wa gazeti la upekuzi la Red Pepper, Juice FM na gazeti linalochapishwa kwa lugha ya kiganda la ‘Kamunye,’ nao wanakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuipindua serikali ya rais Yoweri Museveni.
Vituo hivyo vimefunguliwa hivi majuzi baada ya kufungiwa kwa mda wa mwezi mmoja kwa makosa ya kuandika habari za kichochezi na zenye lengo la kuvuruga amani nchini humo.
Chanzo:VOA
Share To:

msumbanews

Post A Comment: