Katibu Tawala wa Wilaya ya Arumeru Bw Timotheo Mnzava amemtaka Mtendaji wa Mamlaka ya mji mdogo wa Ngaramtoni kuchukua haraka hatua dhidi ya watu waliojenga pembeni ya vyanzo vya maji na wanaotapishia na kutiririsha maji taka katika mifereji na chem chem ambazo wananchi wengine wanatumia maji yake kwa shughuli za kibinadamu.

"Siku za nyuma baadhi ya nyumba na vyoo viliwekwa alama ya X lakini naambiwa zilikuja kufutwa kinyemela. Lazima sasa mchukue hatua, haiwezekani mtu akaweka choo cha shimo hapa kwenye ukingo wa mfereji wa maji yanayotumiwa na watu wengine majumbani na viongozi na wataalam mpo"

Katibu Tawala alitoa agizo hilo wakati alipofika na kujionea nyumba na vyoo vilivyojengwa pembeni ya mfereji na chem chem ya maji katika Kata ya Moivo, halmashauri ya Arusha vijijini ndani ya wilaya ya Arumeru.

Katika hatua nyingine amewataka wataalam wa mamlaka ya mji mdogo wa Ngaramtoni kuchunguza kibali cha ujenzi cha mkazi mmoja ambaye ndani ya eneo lake lenye uzio kuna chem chem  ambayo imezibwa na kufanywa shimo la taka.

"Mimi ninazo taarifa kuwa hata kibali chako cha ujenzi unachosema ulipewa na Halmashauri ya Arusha DC kinaonekana kutolewa mwaka 2007 mwezi march wakati mwezi march halmashauri ya Arusha haikuwa imeanzishwa lakini pia hakina hata namba ya kibali. Wataalam wa mipango miji na ujenzi mkichunguze hicho kinachoitwa kibali ili lakini na umiliki wake kwa ujumla". Alisisiitiza Katibu Tawala
Share To:

msumbanews

Post A Comment: