Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Korea  Song Geum – Young ofisini kwake ambapo kwa pamoja walijadiliana namna bora ya kuisaidia uboreshaji wa Miundombinu ya Hospitali ya Tiba na Taaluma ya Mloganzila.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa  Joyce Ndalichako akizungumza na Balozi wa China Wang Ke kuhusu ufadhili wa masomo katika Sekta ya Afya kutoka Serikali ya China kwa mwaka wa masomo wa 2018/2019 katika ngazi za Uzamili na Uzamivu. 


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichoko ameishukuru Serikali ya Watu wa China kwa kukubali ombi  lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli la kufadhili  wataalam wa sekta ya Afya.


Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo hii leo alipotembelewa na Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke aliyefika katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo kuhusu utaratibu wa kupata wanafunzi watakaofaidika na ufadhili huo.


Balozi Wang Ke amesema baada ya Rais wa China kupata maombi hayo ametoa ufadhili wa Serikali yake kwa wanafunzi 20 wa Kitanzania watakaopata ufadhili wa masomo katika Sekta ya Afya kutoka Serikali ya China kwa mwaka wa masomo wa 2018/2019 katika ngazi za Uzamili na Uzamivu.


Aidha, Balozi Wang Ke amesema mbali na ufadhili huo pia Serikali ya China itaendesha Mpango wa Mafunzo kwa wataalamu wengine 20 mpaka 30 wa Sekta ya Afya kwa muda wa mwezi mmoja nchini China, hivyo amemuomba Waziri  wa Elimu kusaidia katika kuratibu upatikanaji wa Wanafunzi na aina ya mafunzo ambayo yatasaidia katika kutatua changamoto katika Sekta ya Afya.


Katika hatua nyingine Waziri  Ndalichako amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea Song Geum – Young  kwa lengo la kujadili ujio wa wabunge kutoka Bunge la Korea kwa ajili ya kutoa msaada katika Hospitali ya Tiba na Taaluma ya Mlongazila.


Waziri Ndalichako amemwambia balozi huyo kuwa Serikali bado inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga mbiundombinu ya kuwezesha wanafunzi na wauguzi kuishi karibu na hospitali ya Taalum na Tiba ya Mlongazila.


Waziri amesema kwa sasa serikali ipo katika ujenzi wa awamu ya kwanza ya Miundombinu itakayowezesha wanafunzi wapatao 1500 kuishi karibu na hospitali hiyo.


Waziri Ndalichako amesema Hospitali hiyo imejengwa kwa lengo la kuongeza udahili wa wanafunzi mpaka kufikia wanafunzi zaidi ya 10,000 hivyo bado Miundombinu itakayowezesha kuchukua idadi hiyo ya wanafunzi pamoja na watumishi wa hospitali hiyo inahitajika.


Naye Balozi wa Jamhuri ya Korea amesema serikali yake bado itaendelea kusaidia katika uendeshaji wa hospitali hiyo pamoja na miradi mingine katika Sekta ya Elimu.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

26/2/2018                             
Share To:

msumbanews

Post A Comment: